Joy FM

Elvee Mediwear Charity imetoa viti mwendo kwa wanafunzi wenye uhitaji Kasulu

24 November 2025, 13:01

Ni muonekano wa watoto wenye ulmavu wakiwa kwenye viti mwendo vilivyotolewa, Picha na Hagai Ruyagila

Jamii na wadau wa maendeleo wameshauriwa kuendelea kujtokeza na kuwasaidia watoto wenye ulemavu ili waweze kujiona ni sehemu ya jamii

Na Hagai Ruyagila

Katika kuunga mkono jitihada za serikali kwa kuboresha sekta ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum, Kampuni ya Elvee Mediwear Charity kutoka Marekani tawi la Dar Es Salaam imetoa viti mwendo viwili kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji katika Shule ya Msingi Kalema Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma. Viti hivyo vimekabidhiwa kupitia kwa Mwl. Yusuph Ibrahim.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mwl. Yusuph Ibrahim kutoka Shule ya Msingi Kisuma, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, amesema mbali na kukabidhi viti mwendo hivyo, pia Taasisi ya USILIE TENA kutoka Dar Es Salaam imewasaidia watoto 23 kwa kuwakatia bima za afya, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wanafunzi wote wanapata huduma muhimu za kijamii.

Baadhi ya watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Kalema halmashauri ya Mji Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Amewataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha watoto wao na badala yake waendelee kuwalea na kuwathamini ili wapate haki sawa ya elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.

Sauti ya Mwl. Yusuph Ibrahim kutoka Shule ya Msingi Kisuma, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Salvatory Kitogwe, amesema serikali inaendelea kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye mahitaji maalum kwa kushirikiana na taasisi binafsi ili kuhakikisha wanapata haki ya elimu bila vikwazo, jambo ambalo litawasaidia katika kujitengenezea mustakabali bora wa maisha.

Sauti ya Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Salvatory Kitogwe
Mwl. Salvatory Kitogwe mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Mwakilishi wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kalema, Bi. Mary Hulilo, amewasisitiza wazazi kuvitunza viti hivyo ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu na kuboresha mazingira yao ya kujifunzia.

Sauti ya Mwakilishi wa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kalema, Bi. Mary Hulilo

Wazazi wa watoto waliopokea viti mwendo wameishukuru Taasisi ya Elvee Mediwear kwa moyo wa upendo na kujali watoto wao ambapo wamesema msaada huo utasaidia kuongeza ushiriki wa watoto wao katika masomo na shughuli mbalimbali za kila siku shuleni.

Sauti ya Wazazi wa watoto waliopokea viti mwendo wameishukuru Taasisi ya Elvee Mediwear kwa moyo wa upendo na kujali watoto