Joy FM

Miche 200,000 ya kahawa yagawiwa kwa wakulima Kasulu

18 November 2025, 17:16

Wananchi wa kata ya Buhoro wakiwa na watalamu wa kilimo katika kuendelea kuhamasishwa kujikita katika kilimo cha Kahawa, Picha na Emmanuel Kamangu

Wakulima katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kujikita katika kilimo cha kahawa ili waweze kujikwamua kiuchumi

Na Emmanuel Kamangu

Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma leo Jumanne Novemba 18, 2025, imetoa jumla ya miche 200,000 ya Kahawa aina ya robusta kwa wakulima, ikiwa ni hatua ya kuhamasisha kilimo cha kibiashara ili kuongeza uzalishaji na kuwawezesha wananchi kunufaika zaidi na zao hilo.

Akizungumza katika tukio hilo lililofanyika katika Kata ya Buhoro, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, CPA Francis Kafuku, amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kutokana na miche hiyo kutolewa bure pasipo gharama yoyote.

Aidha CPA Kafuku amesema mikoa ya kaskinizini miche hiyo hutolewa kwa gharama kubwa hivyo kuna kila sababu ya wananchi kuona nia na dhamira ya serikali ya Rais  Dkt samia suluhu Hassani ya kuhakikisha wananchi wanajikita katika kilimo cha biashara ili kujikwamua kiuchumi.

Mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya kasulu Bw, Francis Kafuku, Picha na Emmanuel Kamangu

Kwa upande wake, Diwani Mteule wa Kata ya Buhoro, Charles Kinele, amesema mbali na wananchi wengi wa eneo hilo kujikita zaidi katika kilimo cha chakula bado kuna kila sababu za kuingia katika kilimo cha biashara ambacho kitakuwa rahisi kuwavusha kimaendeleo.

Awali, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo, Mikidadi Mbaruku amesema kuwa uzalishaji wa miche hiyo unafanyika kwa ushirikiano na bodi ya Kahawa, ambapo Halmashauri hutenga eneo kwa ajili ya vitalu vya miche huku akiwashukuru wananchi kwa kushiriki kikamilifu kuilea hadi hatua ya kupelekwa shambani.

Hata hivyo baadhi ya wakulima kutoka kijiji cha heru ushingo Bi. Noadia Konge amesema atahamasisha wakulima wenzake, hususan wanawake, kujiunga kwenye kilimo cha kahawa ili kwenda sambamba na mfumo wa kilimo chenye tija ambacho serikali imekuwa ikikisisitiza.