Joy FM

Zaidi ya miche milioni 1.3 ya kahawa yagawiwa kwa wakulima Kasulu

17 November 2025, 15:32

Muonekano wa miche ya Kawaha iligawiwa kwa wananchi Halmashauri ya Mjii Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu imewataka wakulima kutunza vizuri miche ya kahawa waliyopewa ili iweze kuwanufaisha na kuongeza kipato cha familia na Taifa kwa ujumla

Na Hagai Ruyagila

Zaidi ya miche Milioni 1.3 ya Kahawa imegawiwa kwa wakulima zaidi ya 1000 katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma kwa lengo la kukuza na kuendeleza kilimo cha zao la Kahawa katika halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mratibu wa zao la Kahawa Halmashauri ya Mji Kasulu Eliakimu Charles amesema idadi ya maombi ya miche kutoka kwa wakulima ilikuwa kubwa kuliko miche iliyoandaliwa, amefafanua mwitikio huo mkubwa unatokana na elimu ya kilimo bora cha kahawa iliyotolewa na serikali kuhusu manufaa ya zao hilo kimapato na kiuchumi.

Sauti ya Mratibu wa zao la Kahawa Halmashauri ya Mji Kasulu Eliakimu Charles
Mratibu wa zao la Kahawa Halmashauri ya Mji Kasulu Eliakimu Charles, Picha na Hagai Ruyagila

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye amesema ugawaji wa miche hiyo ni zoezi endelevu kwani serikali imeweka mkazo katika kumwezesha mkulima na kuhakikisha ananufaika kikamilifu na kilimo cha kahawa.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amewataka wakulima kuhakikisha wanapanda miche hiyo ndani ya Halmashauri hiyo na kuitunza ipasavyo ili iweze kuwanufaisha.

Aidha amebainisha kuwa serikali iko tayari kuwatafutia masoko wakulima hao ili kuhakikisha mazao yao yanapanda thamani inayostahili.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu akigawa miche ya kahawa kwa wakulima, Picha na Hagai Ruyagila
Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu

Baadhi ya wakulima wa zao hilo katika halmashauri ya Mji Kasulu wamesema kahawa imeendelea kuwa na manufaa makubwa katika kukuza uchumi wao na kuwasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku.

Sauti ya wakulima wa zao la Kahawa