Joy FM
Joy FM
7 November 2025, 09:10

Mkuu wa Mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Manispaa ya Kigoma ujiji kupitia kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha huduma ya choo inapatikana katika soko la Nazareti
Na Mwandishi wetu
Wafanyabiashara katika soko la wakulima la Nazareti lililoko Manispaa ya Kigoma Ujiji wamelalamikia kukosa huduma ya choo na maji katika soko hilo kwa zaidi ya miaka miwili sasa hali ambayo inaathiri usafi ndani ya soko hilo.
Wafanyabiashara hao wametoa malalamiko hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, wakati alipotembelea sokoni hapo kwa lengo la kukagua mwenendo wa shughuli za kibiashara na kukuta biashara zikiendelea kama kawaida.

Hata hivyo wafanyabiashara katika soko hilo wameeleza keo mbali mbali za kibiashara na kijamii ikiwemo huduma ya choo na ukosefu wa huduma ya maji wakieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikiwaletea usumbufu mkubwa na hata kuhofia magonjwa ya mlipuko.
Kufuatia malalamiko hayo na baada ya yeye mwenyewe kujionea hali ilivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Sirro, ameelekeza kuchukuliwa kwa hatua za haraka za ujenzi wa choo pamoja na kuwekwa huduma ya maji ndani ya soko hilo.