Joy FM

Jeshi la zimamoto Kigoma lapata mitambo mipya

24 October 2025, 17:26

Mkuu wa Mkoa Kigoma akizungumza wakati wa hafla kukabidhi vifaa kwa jeshi la zimamoto, Picha na Orida Sayon

Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Kigoma limepokea mtambo wa kisasa wa kuzima moto na vitendea kazi vitakavyowezesha kuboresha upatikanaji wa huduma za zimamoto kwa wananchi.

Na Orida Sayon

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amekabidhi magari manne yaliyotolewa na serikali kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma huku akitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa wakati  kuhusu uwepo wa matukio ya ajali za moto na matukio mengine yanayoshughulikiwa na jeshi hilo.

Amesema, mara baada ya kupokea vitendea kazi hivyo, jeshi hilo linapaswa  kuongeza ufanisi kiutendaji kazi huku akisisitiza utunzaji wa magari na vifaa vingine vilivyopokelewa ili viweze kufanya kazi kwa muda mrefu.

Gari la kuzima moto lililotolewa na serikali, Picha na Orida Sayon

“Pamoja na ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha, Jeshi hili limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kupata mafanikio makubwa kila ilipohitajika kufanya hivyo. Nichukue fursa hii kuwapongezeni kwa kazi nzuri mnazofanya” amesema Sirro.

Aidha Balozi Sirro ameishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji  wa vitendea kazi hivyo, jambo litakaloimarisha utendaji kazi wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa kwenye picha ya pamoja na askari wa jeshi la zimamoto akiwa amevaa vazi la uokoaji, Picha na Orida Sayon

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa ametoa rai kwa Jeshi hilo kutumia vyombo hivyo kwa lengo la kuleta mapinduzi katika eneo lao la utendaji kazi wao.

Amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wa jeshi hilo watahakikisha nyenzo hizo zinatumika kwa kuzingatia malengo ya serikali.

Gari la kuzima moto lililotolewa na Serikali, Picha na Orida Sayon

Awali akitoa taarifa ya mapokezi ya vifaa hivyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma Michael Maganga, amesema vitendea kazi walivyopokea ni pamoja na mtambo wa kisasa wa kuzima moto, gari la kubeba maji, gari la operesheni na gari la wagonjwa.

Ametoa wito kwa wananchi mkoani hapa kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa mapema ili liweze kufika maeneo ya matukio kwa wakati jambo litakalofanikisha kupunguza athari za majanga.