Joy FM
Joy FM
8 October 2025, 13:08

Serikali kupitia Idara ya Kilimo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imewataka wananchi kuhakikisha wanawekeza katika kilimo cha pamba ili kujiongezea kipato kwa familia na taifa kwa ujumla.
Na Hagai Ruyagila
Wananchi wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuwekeza nguvu katika kilimo cha zao la pamba kufuatia jitihada za serikali za kuboresha sekta hiyo, ikiwemo utoaji wa pembejeo kama mbegu bora, lengo likiwa ni kuongeza tija na kuinua uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya pamba duniani yaliyofanyika jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Asantenyerere, kata ya Asantenyerere, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi rasmi wa msimu mpya wa kilimo cha pamba kwa mwaka wa kilimo 2025/2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Mwakisu amesema kuwa serikali inaendelea kumjali mkulima wa pamba kwa kuliendeleza zao hilo ambalo ni la kimkakati na lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla huku akiwasisitiza wananchi kulitilia mkazo zao hilo kwa kulima kwa tija na kufuata kanuni bora za kilimo.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kasulu, Michael Kihiga, amezungumzia mafanikio yaliyopatikana katika zao hilo kwa msimu wa kilimo uliuopita pamoja na mikakati iliyowekwa kwa ajili ya kumsaidia mkulima kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba.

Baadhi ya wakulima wa pamba, akiwemo Edisa Lutogwa, wameishukuru serikali kwa namna inavyowajali wakulima hao, lakini pia wamebainisha changamoto zinazowakabili, zikiwemo upungufu wa pampu za kupulizia viuatilifu dhidi ya wadudu waharibifu.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo wakulima, viongozi wa serikali, wataalamu wa kilimo na mashirika ya maendeleo, ambapo elimu juu ya fursa zilizopo katika kilimo cha pamba imetolewa pamoja na kuhamasisha jamii kuchangamkia zao hilo muhimu kiuchumi.