Joy FM

MCT yanoa wanahabari kukabiliana na habari potofu Kigoma

8 October 2025, 11:39

Meneja Programu Baraza la habari Tanzania (MCT) Josephati Mwanzi akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari Kigoma, Picha na Tryphone Odace

Baraza la habari Tanzania (MCT) limetoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari Mkoani Kigoma yenye lengo la kupambana na changamoto za habari na taarifa potofu, na mwongozo wa sheria kuhusu upatikanaji wa taarifa na ushiriki wa taasisi za Serikali katila upatikanaji hasa kipindi cha uchaguzi.

Na Tryphone Odace

Waandishi wa habari Mkoani Kigoma wameaswa kuhakikisha wanaandika taarifa zenye ukweli na usahihi ili kuepuka kuandika habari zenye kuposha na kuleta taharuki kwenye jamii.

Hayo yamebainishwa na Meneja Programu kutoka Baraza la habari Tanzania (MCT) Josephati Mwanzi  wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari Mkoani Kigoma na wadau mbalimbali kilichofanyika  Oktoba 8, 2025.

Amesema wananchi wamekuwa hawapati taarifa sahihi na hivyo jamii kukosa taarifa zenye usahihi na zinazochochea maendeleo kwa jamii kwa sababu ya uwepo taarifa nyingi ambazo hazina usahihi na hivyo kuwataka wanahabari kuwa mstari wa mbele kuandika taarifa ambazo zinaisaidia jamii kupata habari zenye usahihi.

Waandishi wa habari Mkoani Kigoma wakiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Polisi wakati wa mafunzo ya MCT, Picha na Tryphone Odace

Bw. Mwanzi amesema wanahabari ni nguzo muhimu katika kuunganisha jamii na mamlaka na kuwa  hawana budi kuhakikisha wanaandika habari zinazochochea upendo, amani na mshikamano wa jamii na taifa kwa ujumla.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, Mkuu wa Wilaya Kigoma Dkt.Rashid Chuachua amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kufuata kanuni na kisheria za habari ili kuhakikisha hawaandiki taarifa ambazo zinaweza kuleta taharuki na kusababisha uvunjifu wa amani kwa jamii na taaifa.

Mkuu wa Wilaya Kigoma Dk. Rashid Chuachua akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Picha na Tryphone Odace

Aidha Dkt. Chuachua amewataka wanahabari kutokubali kutumika kisiasa na badala yake watoe fursa sawa kwa  wanasiasa wakati wa kuripoti habari zao hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao utarajiwa kufanyika oktoba 29, 2025.

“Tuko katika kipindi ambacho wanasiasa wanaendelea na kampeni za uchaguzi mkuu niawaase wanahabari msikubali kutumika kisiasa na mkasahau wajibu wa kuhabarisha umma taarifa zenye ukweli na wapeni mizania sawa wagombea ili kusiwepo na suala la kuegemea upande wa mgombea mmoja pekee” amesema Dk.Chuachua.

Hata hivyo amewataka waajiri na wamiliki wa vyombo vya habari kuajiri wanahabari wenye taaluma ya habari ili kusaidia kuondoa watu wasiokuwa na elimu ya habari kuendelea kuandika habari bila weledi na matakwa ya sheria ya habari.

Baadhi ya waandishi wa habari Mkoani Kigoma kutoka vyombo mbalimbali wamesema kuwa watahakikisha wanaandika na kuripoti habari zenye maslahi kwa umma ili kusaidia kuchochea maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla na kuhakikisha wanahakiki taarifa zao kabla ya kuzichapisha.

Baadhi ya waandishi wa habari Mkoani Kigoma na wadau mbalimbali wakiwemo Jeshi la Polisi Kigoma wakiwa katika mafinzo yaliandaliwa na MCT, Picha na Tryphone Odace