Joy FM

Zitto kuboresha barabara na soko kata ya Businde Kigoma

24 September 2025, 08:55

Wananchi na wanachama wa chama cha ACT – Wazalendo wakiwa katika mkutano wa kampeni za Zitto Kabwe, Picha na Tryphone Odace

Chama cha ACT- Wazalendo kimesema kuwa kimedhamiria kuhakikisha kinaboresha maisha ya wananchi wa Kata ya Businde kwa kujenga barabara, Soko na kutatua changamoto zinazowakabili ili kata hiyo ionekane kama kata iliyopo ndani ya Manispaa

Na Tryphone Odace

Mgombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini, kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema akishinda ubunge katika Jimbo hilo atahakikisha anafungua Kata ya Businde kwa kuweka barabara za kuingia na kutoka ili wananwanchi waweze kunufaika na shughuli za usafiri na usafirishaji.

Akizungumza leo Jumanne, Septemba 23, 2025 katika mkutano wa kampeni uliyofanyika Kata ya Businde Manispaa ya Kigoma Ujiji, Zitto amesema kutokana na ubovu wa barabara ya kata hiyo wananchi hutumia gharama kubwa za  usafiri kuanzia Shilingi 4,000 kwenda mjini kufanya shughuli zao kwa bodaboda wakati wananchi wa maeneo mengine yaliyopo nje ya mji wakitumia shilingi 1000 kusafiri hadi mjini.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe akihutubia katikamkutano wa kampeni kata ya Businde, Picha Tryphone Odace

Amesema wakichukua Halmashauri jambo la kwanza ni kuhakikisha wanawekeza miundombinu ya barabara katika kata pamoja na kurudisha mradi wa barabara ya Kasulu kupitia Msimba –Ujiji, ambao kwa kipindi chake aliuanzisha na kuomba fedha kutoka Benki ya Dunia.

Sauti ya Mgombea ubunge Zitto Kabwe

Naye Mgombea udiwani kata ya Businde, Said Makala amesema wananchi wasidanganyike kwani wananchi hao wanajua uwezo wake wa utendaji kazi hasa katika utatuzi wa changamoto za wananchi na kuchochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Katibu wa chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Yunus Luhovya amesema chama hicho kilipokuwa kinaongoza halmashauri hiyo kiliweza kufanya maendeleo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami.

 Kwa upane wake, Mwenyekiti wa ngome ya vijana wa chama cha ACT – Wazalendo Abdull Nondo amesema kuwa miongoni mwa vitu ambavyo vimekuwa vikikwamisha Kigoma kusonga mbele kwenyesuala la maendeleo ni pamoja na kukosa viongozi thabiti wa kuweza kuwatetea wananchi kama ambavyo alikuwa akifanya Zitto Kabwe kipindi yupo madarakani

Mwenyekiti wa ngome ya vijana wa chama cha ACT – Wazalendo Abdull Nondo, Picha na Tryphone Odace

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Businde Manispaa ya Kigoma Ujiji, wamesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na barabara, soko, ukosefu wa huduma za afya na viwanja vyao kutokupimwa