Joy FM
Joy FM
18 September 2025, 10:09

Chama cha ACT Wazalendo kimeahidi kuhakikisha kinatatua changamoto zinawakabili wananchi wa Kata ya Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa kuboresha na kuendelea miradi iliyoanzishwa na chama hichi kwa kipindi walichokuwepo madarakani ikiwemo barabara na maji
Na Mwandishi wetu
Mgombea ubunge kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe amesema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha anaanzisha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa watu wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya pamoja na uboreshaji wa barabara na maji.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za chama hicho na wananchi wa kata ya Kagera Manispaa ya Kigoma Ujiji, Zitto Kabwe amesema kumekuwepo na ukosefu huduma bora za afya na maji jambo ambalo linasababisha wananchi washindwe kufanya kazi kwa ufanisi.

Amesema ili kurahisisha shughuli za usafirishaji kwa wananchi wa kata ya kagera watahakikisha wanajenga barabara na daraja.
Aidha amesema kuwa watahakikisha wanaendeleza mradi wa umwagiliaji wa mto Luuiche ili uweze kuwanufaisha wananchi na kuifanya kata hiyo kuwa eneo la kimkakati.
Baadhi ya wananchi wa kata ya kagera wameomba mgombea huyo wa Ubunge kuwasaidia kulipwa fidia kwa wananchi waliobomolewa nyumba zao na kuhakikisha anatatua changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili ikiwemo ukosefu wa vitambulisho vya Taifa NIDA na mikopo kwa vijana.

Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea na kampeni katika maeneo mbalimbali na kueleza sera zake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktaoba 29 mwaka huu.