Joy FM

Dkt. Samia kutua Kasulu Septemba 13

10 September 2025, 14:18

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Bi. Jenifer Chinguile, Picha na Hagai Ruyagila

Wananchi wa Wilaya ya Kasulu wameeleza furaha yao kwa ujio wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mgombea Urais kuwa utatoa nafasi kwa wananchi kueleza mahitaji yao

Na Hagai Ruyagila

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya ziara katika Wilaya ya Kasulu mnamo tarehe 13 Septemba mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Bi. Jenifer Chinguile, amesema ujio wa Dkt. Samia unalenga kunadi sera za chama hicho kwa wananchi, ili kuwaomba tena ridhaa ya kuongoza taifa kwa kipindi kingine.

Sauti ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Bi. Jenifer Chinguile

Bi, Chinguile ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia imefanya mambo mengi makubwa katika Wilaya ya Kasulu, ikiwemo miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, barabara, na maji safi na salama.

Aidha, wananchi wa Wilaya ya Kasulu wameeleza furaha yao kwa ujio wa Rais ambaye pia ni mgombea urais, wakisema kuwa utatoa nafasi kwa wananchi kueleza mahitaji yao na kuonesha maeneo ambayo bado yanahitaji msukumo wa maendeleo.

Wananchi hao wamesema kuwa ujio wa Dkt. Samia utawapa fursa ya kusikilizwa moja kwa moja na kiongozi mkuu wa nchi, jambo ambalo linaongeza imani yao kwa chama na serikali kwa ujumla.

Mmojawa wananchi wa Wilaya ya Kasulu wakizungumzia ujio wa Dkt. Samia, Picha na Hagai Ruyagila

Ziara hiyo inatarajiwa kuwa ya kihistoria kwa wakazi wa wilaya ya  Kasulu, huku ikilenga kuimarisha mshikamano kati ya chama na wananchi katika kuelekea uchaguzi mkuu.