Joy FM

DC Kasulu ataka wananchi kushiriki kampeni za uchaguzi

4 September 2025, 15:27

Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali imewataka wananchi Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma kushiriki katika uchaguzi na kuwapata viongozi wataoweza kuwasaidia kutatua changamoto zao

Na Hagai Ruyagila

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Kanal Isaac Mwakisu amewataka wananachi wa Wilaya hiyo kushiriki kikamilifu katika kampeni za wagombea mbalimbali wa nafasi za uongozi ili kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo katika maeneo yao.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika uwanja wa Umoja uliopo Mjini Kasulu.

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanal Isac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila

Kanal Mwakisu amesema kampeni za uchaguzi tayari zimezinduliwa rasmi hivyo ni muhimu kwa wananchi kuhudhuria mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera na mipango ya wagombea kabla ya kufanya uamuzi wa nani anafaa kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Kanal Isaac Mwakisu

Kwa upande wake, Mchungaji wa kiongozi wa Kanisa la CGRA Murusi Dickison Nyandura amewahimiza wananchi wa dini zote kuendelea kuliombea taifa ili liendelee kuwa na amani.

Pia amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa kwa utulivu, haki na uwazi hali itakayochangia kupatikana kwa viongozi wenye maono, hekima na uzalendo wa kweli katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Sauti ya Mchungaji wa kiongozi wa Kanisa la CGRA Murusi Dickison Nyandura

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kasulu wamesema wako tayari kushiriki kampeni kwa makini ili kuwachunguza wagombea na kufahamu yupi anaweza kuwatumikia kwa uadilifu, na hatimaye kufanya uamuzi sahihi katika uchaguzi ujao sambamba na kuendelea kuombea uchaguzi huo.

Sauti ya baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kasulu

Mchakato wa kampeni unaendelea kote nchini, huku viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali wakihimiza ushiriki wa wananchi katika hatua zote muhimu za uchaguzi ili kupatikana viongozi bora wanaoendana na mahitaji ya maendeleo ya jamii zao.