Joy FM
Joy FM
4 September 2025, 15:09

Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi zilizo Mashariki na Kusini mwa Afrika zilizopiga hatua kubwa katika udhibiti wa utakasishaji fedha haramu na uzuiaji wa silaha za maangamizi na ufadhili wa ugaidi nchini.
Na Tryphone Odace
Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali Mkoani Kigoma yametakiwa kuwa makini na kuepuka kutotumiwa vibaya watu wenye nia mbaya na kuingia katika kashfa za utakatishaji fedha haramu na ugaidi ili kusaidia kutoliingiza taifa katika migogoro na machafuko.
Katika ulimwengu wa leo, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanachukuliwa kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na hata kisiasa.
Hata hivyo, yapo baadhi ya mashirika yanayohusika au kutumiwa vibaya kwa shughuli haramu kama vile utakatishaji wa fedha na kufadhili ugaidi na vitendo hivi vinatajwa kuwa na athari kubwa siyo tu kwa serikali bali pia kwa jamii nzima.

Akizungumza na viongozi wa dini na mashirka yasikuwa ya kiserikali Mkoani Kigoma, Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Julias Msengeli amesema utakatishaji wa fedha haramu na ugaidi kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali ni tishio kubwa kwa maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.
Naye Kamishna Msaidizi kutoka kitengo cha fedha haramu Seif Omary Khaji amesema taasisi zisizo za kiserikali zimekuwa zikitumiwa na wahalifu na kupoteza lengo la kuanzishwa kwake ikiwemo kuhudumia jamii.
Katibu tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa anawakumbusha wamiliki wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kutambua wajibu wao ikiwmo kufuata sheria za mashirika hayo.
Baadhi ya wadau wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wameeleza umuhimu wa mafunzo hayo ili kuhakikisha hayawi sehemu ya uvunjifu wa sheria.
Ni jukumu la serikali, vyombo vya usalama, jamii na mashirika yenyewe kuhakikisha kuwa taasisi hizi hazitumiki kama chombo cha uhalifu. Ufuatiliaji, uwazi, na ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kupambana na changamoto hii hatarishi ya utakatishaji fedha na ugaidi.
Hata hivyo, Tanzania imetajwa kuondolewa kwenye Orodha ya nchi zenye mapungufu ya kimkakati katika mifumo ya udhibiti utakatishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa silaha za maangamizi.