Joy FM
Joy FM
18 August 2025, 08:49

Wafugaji wanatarajia kunufaika na uzalishaji wa chumvi lishe kwa ajili ya mifugo na kuongeza thamani ya mifugo na kunufaika na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Na Tryphone Odace
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa hatua ya kiwanda cha chumvi cha Nyanza Mines kilichopo Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma kuendelea kufanya maboresho ikiwemo upanuzi wa kiwanda hicho itasaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi na kuacha kutegemea chumvi kutoka nje ya nchi.
Waziri Mavunde amesema hayo alipotembelea kiwanda cha Nyanza Mines kilichopo wilayani uvinza mkoani kigoma na kuzindua chumvi lishe kwa ajili ya mifugo na kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kipato kwa Taifa.
Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha inatumia rasilimali zilizopo na kuacha kutegemea chumvi kutoka nje na kuwa kiwanda hicho kuanza kuzalisha chumvi lishe kwa ajili ya mifugo ni hatua kubwa na kuungwa mkono kwa manufaa ya mifugo nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya Uvinza Dinnah Mathamani amesema kupitia kiwanda hicho cha kuzalisha chumvi ya mifugo itachochea na kuongeza thamani ya mifugo na kuweza kuuzwa ndani na nje ya nchii.
Kwa upande wake, Ben Mwaipopo Mkurugenzi Mkaazi wa kiwanda cha Nyanza Mines amesema uboreshaji wa kiwanda hicho kumeongeza uzalishaji kutoka tani elfu 9 hadi tani elfu 75 kwa mwaka huu baada ya kufanyika kwa uwekezaji.