Joy FM
Joy FM
6 August 2025, 13:43

Neema yawashukia wamiliki na madereva wa pikipiki baada ya Serikali kueleza kuwa imeondoa kodi kwa vyombo hivyo
Na Timotheo Leonard
Serikali imeondoa kodi ya mapato ya shilingi laki moja na elfu ishirini kwa mwaka kwa vyombo vya pikipiki maarufu kama bodaboda ili kuwapa fursa ya kuinua uchumi wao.
Hayo yamebainishwa na Hamad Iddy Mterry, Afisa Mkuu wa usimamizi wa kodi kutoka mamlaka ya mapata Tanzania TRA, wakati akizungumza na Redio Joy fm kuhusu mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi yaliyofanyika kupitia sheria ya fedha mwaka 2025
Amesema malengo ya serikali kutoa msamaha wa kodi hiyo kwa vyombo vya pikipiki ni kutaka kuwapa nafasi ya kukuza shughuli zao na kuwataka watendaji wa serikali kusimamia ipasavyo.
Baadhi ya madereva wa pikipiki wa kata ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji, wameishukuru serikali kwa kuondoa kodi hiyo huku wakisema itawasaidia kukua kiuchumi.
Aidha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi yaliyofanyika kupitia sheria ya fedha mwaka 2025 ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa.