Joy FM
Joy FM
29 July 2025, 11:39

Wafanyabiashara ya kuvuka mipaka katika Mkoa wa Kigoma, wamezipongeza idara za serikali zinazosimamia taratibu za biashara zote za mipakani kwa kurahisisha mazingira ya biashara hatua ambayo imesaidia kupungua kwa baadhi ya vikwazo vilivyokuwa vinalalamikiwa na wafanyabiashara ikiwemo upatikanaji wa haraka wa huduma za vibali vya kusafirisha bidhaa nje ya nchi na tozo.
Wakizungumza katika kikao cha kupata taarifa ya vikwazo vilivyofanyiwa kazi kwa lengo la kurahisisha biashara za mipakani, baadhi ya wafanyabiashara wamesema kupungua kwa tozo na kusogea kwa idara hizo katika maeneo ya mipaka kumepunguza gharaza za kufanya biashara pamoja na kuwapunguzia muda wa kushughulikia nyaraka zote muhimu kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zao.
Mkaguzi kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania TPHPA, kitengo cha afya ya mimea na viuatilifu forodha ya Kibirizi, Mariam Thobias Mkentimba, na Meneja wa Kanda wa Shirika la Viwango Tanzania TBS, wameeleza namna taasisi zao zilivyorahisisha mazingira ya biashara za mipakani.
Katibu Mtendaji wa TCCIA mkoa wa Kigoma Prosper Guga amesema hayo ni mafanikio makubwa yaliyotokana na jitihada zilizofanyika za kuhakikisha kuwa taasisi za serikali zinazosimamia biashara za mipakani zinakuwa na ofisi zake katika mkoa wa Kigoma ili kutoa huduma kwa wafanyabiashara.
Kikao hicho kimeitishwa na Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo TCCIA mkoa wa Kigoma, ambao wanatekeleza mradi wa kukuza biashara ya mazao ya kilimo kwa wanawake na vijana wakishirikiana na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki, kwa ufadhili wa AGRA.