Joy FM
Joy FM
10 July 2025, 11:50

Serikali imeahidi kuendelea kutoa mikopo kwa makundi ya watu wenye ulemavu, vijana na wanawake wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Na Hagai Ruyagila
Watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmashauri mbali mbali nchini kwa Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl. Vumilia Simbeye wakati akizungumza na radio Joy Fm Mjini Kasulu.
Amesema kumekuwepo na changamoto hasa kwa watu wenye ulemavu kutojitokeza kuomba mkopo wa asilimia kumi inayotolewa na serikali katika mapato yake ya ndani ili iweze kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kupata maendeleo yatakayowasaidia kufanikisha ndoto zao.
Aidha Mwl, Simbeye ameendelea kuwahamasisha Vijana, Wanawake na Wenyeulemavu kutumia fursa za mikopo ya serikali ya asilimia kumi kwa ajili ya kufanikisha maono yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenyeulemavu Wilaya ya Kasulu Zakayo Nkohozi amesema ni vizuri serikali ikatoa elimu ya fedha hizo za asilimia kumi kwa watu wenyeulemavu ili nao wawe na elimu ya namna hiyo.