Joy FM

TANESCO: Mradi wa umeme megawati 49.5 upo 10%

3 July 2025, 11:24

Muonekano wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika Mto Malagarasi Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma, Picha na Mtandao

Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limeendelea kuhakikisha linafikisha huduma ya umeme kwa wananchi

Na Emmanuel Matinde

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limesema kazi ya utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika Mto Malagarasi wilayani Uvinza mkoani Kigoma, unaogharimu Dola za Marekani Milioni 144, sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 400 za kitanzania unaendelea vizuri ambapo hadi sasa umefikia takribani asilimia 10%.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Waandishi wa Habari katika eneo la mradi la Igamba II, ikiwa ni baada ya kukagua na kutoa maelekezo kwa wasimamizi kumsimamia vema mkandarasi atekeleze wajibu wake.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange

Ameeleza kuridhishwa na kazi inayoendelea huku akisisitiza kwamba TANESCO imejipanga vilivyo kufidia muda uliopotea katika hatua za awali za mradi huo, kufuatia dosari kadhaa zilizojitokeza ili kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange

Aidha Bw. Lazaro amesema Mradi wa Kuzalisha Umeme katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma, utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa baada ya kukamilika; Ni mojawapo ya jitihada za serikali za kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosheleza mahitaji ya watanzania.