Joy FM

Mafuriko yanufaisha vijana kwa kuvusha watu Kibirizi

6 May 2025, 12:24

Kijana akiwa anasukuma mtumbwi uliobeba watu wanaovuka kutokana na maji kufunika barabara, Picha na Josephine Kiravu

Licha ya shuruba wanazokutana nazo wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyoathirika mafuriko Katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, baadhi ya vijana wametumia mafuriko hayo kuwa fursa kwa kujipatia kipato kupitia kuwabeba watu wanaovuka.

Na Josephine Kiravu

Baadhi ya vijana katika eneo la kibirizi lililopo Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkoani Kigoma wametumia mafuriko yaliyoikumba barabara ya eneo hilo yaliyotokana na kujaa kwa ziwa Tanganyika kama fursa ya kujipatia kipato kwa kuanzisha biashara ya kuvusha watu kwa mitumbwi.

Ule msemo maarufu usemao kufa kufaana ndio unaodhihirika katika eneo hili la kibirizi.

Kijana akiwavusha wananchi wanaoumia barabara ya kibiri baada ya barabara hiyo kufunikwa na maji Picha na Josephine Kiravu

Eneo hilo hapo awali lilikuwa na barabara sasa limejaa maji jambo ambalo limegeuka fursa kwa vijana hawa akiwemo Japhet Godson na Misigaro Haruna.

Sauti ya vijana wanaovusha watu katika eneo la kibirizi

Wenyewe wanasema shughuli hii inawasaidia kupata kipato kinachosaidia kuendesha maisha yao.

Kwa wakazi wa maeneo haya wanasema licha ya uwepo wa nafuu hiyo bado wanakilio kwa serikali.
Hata hivyo kwa mujibu wa Meneja wa TARURA wilaya ya Kigoma Mhandisi Elias Mtapima amesema tayari barabara hiyo ya kibirizi na Kagashe Road zipo kwenye mpango wa kufanyiwa ukarabati na kuwashauri wananchi kutumia barabara mbadala ambazo hata hivyo baadhi yao zinahitaji ukarabati

Kwa wengi  mafuriko hubeba uharibifu na usumbufu lakini kwa vijana hawa wa kibirizi yamekuwa daraja la kujiajiri na kujipatia kipato ambacho kinasaidia kuendesha maisha yao.

Kijana akiwavusha wananchi wanaoumia barabara ya kibiri baada ya barabara hiyo kufunikwa na maji, Picha na Josephine Kiravu