Joy FM
Joy FM
2 May 2025, 13:05

Mratibu wa shirikisho wa vyama vya wafanyakazi ameomba Serikali kufanyia marekebisho sheria ya utumishi wa umma ili kuondoa mkanganyiko.
Na Hagai Ruyagila – Kakonko
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, amevitaka vyama vya wafanyakazi kuhakikisha vinazingatia usawa wa haki baina ya waajiri na waajiriwa ili kupunguza migogoro sehemu za kazi.
Andengenye ametoa wito huo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mwenge, wilayani Kakonko, mkoani Kigoma.

Amesema ni muhimu kwa vyama vya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa haki na usawa bila kupendelea upande wowote, ili kulinda amani na ustawi katika mazingira ya kazi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoani Kigoma Jumanne Magulu ameieleza serikali katika risala kuhusu changamoto zinazokabili wafanyakazi na kuiomba kufanya marekebisho ya sheria ya utumishi wa umma ili kuondoa mkanganyiko uliopo kati yake na sheria ya ajira na mahusiano kazini.

Baadhi ya wafanyakazi waliotoa maoni yao wamesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kazini ili kuchochea maendeleo katika maeneo yao ya kazi.
Maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya wafanyakazi Meimosi yamebeba kaulimbiu isemayo uchaguzi mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi sote tushiriki.