Joy FM
Joy FM
24 April 2025, 16:00

Wakati mvua ikiendelea kunyesha na kuathiri miundombinu na makazi ya watu katika eneo la Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji, Baraza la madiwani limeomba juhudi za haraka kuchukuliwa ili kuwasaidia wananchi ambao wameathirika na mafuriko.
Na Orida Sayon
Baraza la madiwani katika manispaa ya Kigoma Ujiji limeitaka halmashauri kuongeza jitihada kunusuru waathirika wa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali katika manispaa ya Kigoma Ujiji
Hayo yamejiri katika kikao cha baraza la madiwani la manispaa ya Kigoma Ujiji wakati wa kuwasilisha taarifa za kata ambapo Diwani wa kata ya katubuka Mh. Moshi Anderson Mayengo amehoji ipi hatima ya wananchi wa eneo hilo huku Mheshimiwa Halima Kibiriti diwani viti maalum akihoji mpango wa serikali kutekeleza ujenzi wa barabara mbadala kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Akitoa majibu ya hoja hizo, Kaimu mkurugenzi manispaa ya Kigoma Ujiji, David Rwazo amesema tayari halmashauri imetenga maeneo kwa ajili ya majanga na kuwaelekeza wananchi kuhama kutoka maeneo yanayoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mbunge wa jimbo la Kigoma Mh. Shaabani Ngenda amesema serikali kuu ipo katika mchakato wa kutatua changamoto ya eneo la katubuka na kwamba waathirika watapata msaada.
Athari za mvua katika eneo la katubuka zilianza kuonekana mnamo mwaka 2023 ambapo zilipelekea kaya nyingi kuvamiwa na maji na watu kuhama makazi yao.