

25 March 2025, 11:28
Madereva wa magari madogo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wameaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Madereva wa magari madogo ya kubeba abiria katika halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia chuo cha taifa cha usafirishaji NIT kwa kuendelea kuwapatia mafunzo ya usalama barabarani ambayo yatawasaidia kupunguza ajari zisizotarajiwa.
Madereva hao akiwemo Adrof Michael na Yekonia Choya wametoa shukrani hizo wakati wakipatiwa mafunzo ya usalama barabarani kutoka kwa wakufunzi wa chuo cha taifa cha usafirishaji NIT.
Wamesema mafunzo hayo ni muhumu kwa madereva wote wa vyombo vya moto ili kuendelea kujua na kutii sheria za usalama barabarani na hivyo kupunguza hatari ya ajari.
Getrude Chale, Mhadhiri Msaidizi kutoka chuo cha taifa cha usafirishaji NIT amesema madereva wa magari madogo ya kubeba abiria wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kusababisha ajari za barabarani, Hivyo mafunzo hayo ni muhimu ili kuwasaidia kuboresha ufanisi wao katika matumizi ya barabara na kuepuka madhara ya ajari.
Kwa upande wake Copro Emmanuel Fussy kutoka jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Kasulu amewasihi madereva hao kutii mafunzo hayo na kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajari na kuhakikisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Naye Mkuu wa kituo cha kikanda cha umahiri katika usalama barabarani (NIT) kanda ya Afrika mashariki na kusini mwa Afrika Godlisten Msumanje amesisitiza kuwa dereva yeyote ana kuwa makini anapoendecha chombo cha moto ili kuepuka ajari.
Mafunzo hayo ya Usalama barabarani Katika halmashauri ya mji Kasulu yameendeshwa na wakufunzi wa chuo cha taifa cha usafirishaji NIT kwa siku tano kwa kushirikiana na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani wilaya ya kasulu yakiwahusisha wanafunzi wa shule za msingi zilizopo kando ya barabara, Madereva wa pikipiki maarufu bodaboda, madereva wa bajaji, madereva wa magari madogo ya kubeba abiria maarufu michomoko na watembea kwa miguu.