Zaidi ya milioni 493 kunufaisha vikundi 21 Kasulu
15 January 2025, 13:00
Halmashauri ya Wilaya Kasulu inatekeleza programu ya mfuko wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kama ilivyo kwa Halmashauri zote nchini kufuatia agizo la Serikali la mwaka 1998 kuwa Halmashauri zote nchini zianzishe mfuko huo kwa kutenga asilimia 10% ya mapato yake ya ndani.
Na Hagai Ruyagila
Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imekabidhi hundi ya mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 493 kwa vikundi 21 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Katika Hafla hiyo ya kukabidhi mikopo ya asilimia 10 ambayo imetolewa katika kipindi cha robo ya pili kuanzia mwezi oktoba hadi disemba 2024/2025 inalenga kunufaisha vikundi 21 vya halmashauri hiyo
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Bw Eliya Kagoma amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya familia zao.
Kagoma amesema serikali itaendelea kuwashika mkono wananchi kuhakikisha wananufaika na mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri ili kuinua uchumi wa jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dkt Semistatus Mashimba amesema mikopo hiyo inalenga kuinua uchumi wa jamii katika kufanya shughuli za maendeleo.
Mkuu wa division ya maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Kasulu Victoria Moses amesema halmashauri inawajibu wa kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa wananchi waliokidhi vigezo na kuwataka kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali na kueleza namna itakavyowasaidia kuendesha maisha yao.