Bilioni 2 kuanza ujenzi wa soko la kimataifa Kagunga Kigoma
24 December 2024, 16:49
Hatimaye Serikali imesaini mkataba wa kuanza ujenzi wa soko la kimkakati katika eneo la Kagunga Halmashauri ya wilaya Kigoma kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi lakini kama sehemu ya kudumisha ujirani mwema kutokana na kuwa soko hilo lipo katika mpaka wa Tanzania na Burundi
Na Tryphone Odace – Kigoma
Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma imesaini mkataba wa kuanza ujenzi wa soko la kimataifa katika kata ya Kagunga ambalo litawezesha wafanyabiashara wa ndani na Nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo kufanya biashara na kukuza uchumi.
Utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa Soko hilo, umeongozwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw. Joseph Nyambwe na kusisitiza mkandarasi aliyepewa tenda ya ujenzi wa soko hilo GOPA CONTRACTERS kuzingatia makubaliano ya mkataba ili mradi ukamilike kwa wakati.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Kigoma Bw. Linus Sikainda amesema hadi kukamilika ujenzi wa soko hilo utakuwa umegharimu shilingi bilioni 5.6, ambapo awamu ya kwanza tayari Serikali imetoa Bilioni 2. Ili kuanza utekelezaji wa mradi huo wa soko.
Aidha Bw. Linus ameongeza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya kuongeza pato la halmashauri na kuwa sehemu ya kitega uchumi kikubwa wa halamshauri.
Kwa upande wake, Mkandarasi aliyepewa Tenda ya Ujenzi wa soko hilo, Godfrey John Mwogera kutoka kampuni ya GOPA CONTRACTERS, mepongeza Serikali kwa kuwaamini wakandarasi wazawa na kwamba ni hatua muhimu kutekeleza miradi kwa ubora na kuhakikisha inaleta chachu ya maendeleo ya jamii na Taifa.