DCP Ramadhani Ng’anzi awataka madereva kutii sheria za usalama barabarani
9 December 2024, 12:26
Madereva wa vyombo vya moto hasa mabasi wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali hasa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Na Josphine Kiravu – Kigoma
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani nchini DCP Ramadhani Ng’anzi amefanya ukaguzi wa mabasi 23 Mkoani Kigoma na kubaini mapungufu kwenye mabasi 3 ambayo yametakiwa kwenda kufanya matenegenezo kabla ya kuendelea na safari.
Akiwa katika eneo la standi kuu ya mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani nchini DCP Ramadhani Ng’anzi ametoa elimu kwa madereva kuhusu madhara ya mwendokasi pamoja na kuwapima kiwango cha ulevi madereva hao huku akiwataka abiria kutokaa kimya wanapoona mwenendo usiofaa kwa madereva.
Nao baadhi ya madereva wa mabasi yaendayo mikoani akiwemo Shabani Kitumbo wamepongeza hatua hiyo ya ukaguzi wa magari na kuwapima madereva kiwango cha pombe mwilini na kulitaka jeshi la polisi kuendelea na zoezi hilo mara kwa mara ili kudhibiti ajali za barabarani.
Kwa upande wao abiria akiwemo Juma Makenzi wamelitaka jeshi la polisi kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara sambamba na kuwapima kiwango cha pombe mwilini kondakta wa mabasi kwani baadhi yao wamekuwa wakitumia pombe kupitiliza.
Mkuu wa jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani nchini ametembelea pia kijiwe cha madereva wa michomoko pamoja na bodaboda huku akiwataka kuzingatia alama za barabarani na kuepuka mwendokasi na kukumbushia ajali mbaya iliyotokea mwaka jana kule Kibondo na kusababisha vifo na majeraha kwa abiria.