Katibu wa siasa uenezi na mafunzo CCM Kigoma atembelea mkurugenzi wa uchaguzi ADC
4 December 2024, 12:16
Siku chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka 2024, Katibu wa siasa, uenezi na mafunzo wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kigoma Deogratius Nsokolo amemtembelea Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwandiga Kaskazini ambaye ndiye mshindi pekee kutoka kwenye vyama vya upinzani.
Na Hamis Ntelekwa – Kigoma
Katibu wa siasa, uenezi na mafunzo wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kigoma Deogratius Nsokolo amemtembelea katika kitongoji chake cha Mwandiga kaskazini katika wilaya ya Kigoma Mkoani Kigoma mwenyekiti wa kitongoji hicho kutoka Chama cha ADC ambaye pia ni mkurugenzi wa uchaguzi wa Chama hicho Taifa Ndg. Mtoro Bakar Mvunye ambaye amechaguliwa Novemba 27 katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na Vitongoji nchini.
Nsokolo amesema amefika katika kitongoji hicho ili kumpongeza mwenyekiti huyo kwa ushindi ikiwa ni mgombea pekee wa chama hicho aliyeibuka mshindi lakini pia ni kiongozi wa kitaifa wa Chama hicho akiwa mkurugenzi wa uchaguzi wa ADC Taifa.
Katika mazungumzo yao Katibu Mwenezi wa Mkoa amemuhakikishia ushirikiano kutoka chama cha Mapinduzi na Serikali katika kuwahudumia wananchi, kulinda usalama wa raia, kusimamia maendeleo ya wananchi, kudumisha upendo na mshikamano na kuwaunganisha wananchi kuwa kitu kimoja.
Amesema mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza juu ya mambo manne ambayo ni Maridhiano, ustahimilivu ,mabadiliko na kujenga upya, hivyo CCM katika mkoa wa Kigoma inayaishi mambo hayo ili kuwafanya Wananchi washirikiane katika maendeleo bila kujali itikadi zao za vyama na kwamba CCM itaendelea kushirikiana na viongozi wote waliochaguliwa kupitia vyama mbalimbali vya siasa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji cha Mwandiga Kaskazini kupitia chama cha ADC Mtoro Mvunye alisema anaiona CCM mpya katika mkoa wa Kigoma kutokana na kutembelewa na kiongozi wa mkoa mara tu baada ya kushinda na kwamba hiyo imempa nguvu katika kuwatumikia wananchi.
“Pamoja na kwamba nimeshinda uchaguzi huu, lakini nilikuwa nawaza namfikishiaje diwani na mbunge wa CCM matatizo ya wananchi wangu, lakini sasa nauona mwanga na kazi yangu itakuwa nyepesi na mimi nitateua wajumbe wa kunisaidia kutoka vyama vyote nilivyogombea navyo ili tushirikiane katika uongozi” alisema Mvunye.
Amesema jambo kubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi ni kushirikiana na kwa kuwa CCM iko tayari na haina kinyongo na ushindi wa upinzani anaamini kitongoji chake na vingine ambavyo wananchi wamefanya uchaguzi na kuchagua upinzani vitapata maendeleo.