Wananchi watakiwa kutoa ushirikiano kwa viongozi wa mitaa Buhigwe
3 December 2024, 14:51
Halmashauri ya Wilaya Buhigwe Mkoani Kigoma kupitia kwa mkurugenzi amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali za mitaa ili waweze kufanya kazi na kuchochea maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Na Emmanuel Kamangu – Buhigwe
Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma wametakiwa kushirikiana na viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 27 mwezi Novemba 2024 ili kuleta maendeleo katika maeneo yao na nchi kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Ndg George Emmanuel Mbilinyi wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa, wazee maarufu na viongozi wa dini wilayani Humo.
Amesema zoezi la uchaguzi limekamilika hivyo ni jukumu la kila mmoja kutoa ushirikiano kwa viongozi waliochaguliwa ili kuhakikisha wanatatua changamoto zilizopo katika jamii.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa Edson Bungwa katibu wa chama cha ACT wazalendo wilaya ya Buhigwe na Dismas John mwenyekiti wa Chama cha CUF Wilayani humo wamesema viongozi waliochaguliwa wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na kutatua kero za Wananchi pasipo kuegemea upande wowote.
Kwa upande wao Viongozi wa dini na wazee maarufu wamesema watahakikisha wanashirikiana na viongozi waliochaguliwa ili kutimiza matakwa ya Wananchi.