NIDA mlango wawekwa wazi kurekebisha taarifa
13 November 2024, 17:35
Wananchi wilayani kasulu mkoani Kigoma ambao wameshapatiwa namba za vitambulisho vya Taifa NIDA wametakiwa kuhakiki usahihi wa majina yao kabla ya kutolewa kwa Vitambulisho hivyo ili waweze kufanyiwa marekebisho kabla ya vitambulisho hivyo kutolewa.
Wito huo umetolewa na Afisa uandikishaji vitambulisho vya Taifa NIDA wilaya ya Kasulu Bw.Peter malale wakati akizungumza na Radio Joy kuhusu umuhimu wa vitambulisho hivyo.
Bw.Malale amesema kumekuwepo na changamoto ya kukosewa kwa baadhi ya Herufi za majina kwenye vitambulisho vya NIDA hali ambayo hupelekea taarifa za majina kukinzana na majina ya vitambulisho vingine na kusababisha usumbufu kwa wananchi wanapohitaji huduma mbalimbali.
Aidha amewataka wananchi kutambua umuhimu wa vitambulisho hivyo kwa kuvitunza ili viweze kuwasaidia katika shughuli mbalimbali pamoja na kutoa taarifa pindi wanapopoteza vitambulisho hivyo ili visiweze kutumika katika uhalifu.