DED Kasulu ahimiza wananchi kutumia muda uliobaki kujiandikisha
18 October 2024, 16:56
Wakati zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la mkaazi kufungwa hapo oktoba 20 mwaka huu, wananchi wametakiwa kutumia muda huo kujitokeza na kujiandikisha ili waweze kupata nafasi ya kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa hapo Novemba 27 mwaka huu.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dr. Semistatus Mashimba amesema zoezi la wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la mpiga kura ndani ya wilaya hiyo linaendelea vizuri licha ya kuwa katika msimu wa kilimo.
Dr. Mashimba amesema hayo wakati akizungumza na radio joy fm ambapo amesema kuwa mwanzoni zoezi lilikuwa na changamoto kwasababu baadhi ya wananchi walijikita kwenye maandaizi ya kilimo ili kuandaa mashaba yao lakini kwasasa zoezi hilo la kujitokeza kujiandikisha linaendeea vizuri kwa wananchi katika vituo vya kujiandikishia.
Aidha Dr Mashimba amesema baadhi ya vijana mwanzoni mahudhurio yao ya kujiandikisha kwenye daftari la mpigakura yalikuwa hafifu lakini kwasasa wameendelea kujitokeza kujiandikisha ili muda utakapofika waweze kuchagua viongozi wao.
Kulingana na tangazo la wizara ya nchi ofisi ya rais, tawala za mikoa na serikai za mitaa TAMISEMI, Mwisho wa wananchi kujiandikisha ni oktoba 20, 2024 na zoezi la kupiga kura itafanyika novemba 27, 2024.