Jamii yaaswa kuacha kuwatumikisha watoto Kasulu
13 September 2024, 14:47
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Uhamiaji wilayani Kasulu mkoani Kigoma Elizabeth George ameitaka jamii kuacha kuwatumisha watoto chini ya umri wa miaka 18.
Na Hagai Ruyagil – Kasulu
Wananchi wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto wenye umri chini ya miaka 18 katika shughuli za kilimo na biashara na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.
Akizungumza na vyombo vya habari, mkaguzi msaidizi wa uhamiaji wilayani Kasulu Elizabeth George amesema hairuhusiwi kumtumia mtoto mwenye umri huo maana kwa kufanya hivyo unakwenda kinyume na sheria za nchi.
Aidha afande Elizabeth amesema endapo unahitaji kumtumia mtu yeyote kutoka nje ya nchi lakini asiye mwenye umri chini ya miaka 18 kwa ajili ya shughuli zozote ikiwemo kilimo ni vizuri kuzingatia sheria zilizopo hasa kwa kufuata kibali cha kufanyia kazi nchini na endapo utaenda kinyume hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wamesema ni vizuri kutomshirikisha mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 maana umri huo anatakiwa kuendelea kupata elimu.
Sambamba na hilo wamesema kwa wale wanaowahitaji watu wa kuwafanyia shughuli za kilimo katika mashaba yao wahakikishe wanafuata vigezo vilivyotolewa na serikali.