Hali ya majeruhi ajali ya treni Kigoma
30 August 2024, 10:46
Majeruhi wa ajali ya treni 73 waliopata ajali wakisafiri kutoka mkoani Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam wanaendelea kupatiwa huduma za matibabu bure chini ya serikali, katika hospitali za wilaya ya Uvinza na Maweni mkoani Kigoma, huku afya zao zikitajwa kuimarika.
Na, Kadisilaus Ezekiel
Ajali ya treni ya abiria ilitokea usiku wa kuamkia Agosti 28 hapo jana, eneo la Lugufu wilayani Uvinza na maejeruhi wameeleza hali zao wakiwa wamelazwa katika hospital ya wilaya ya Uvinza na Maweni mkoa Kigoma ambapo pia Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli nchini TRC Masanja Kadogosa amesema majeruhi wote waliojeruhiwa serikali itagharamikiwa gharama za matibabu na kuwasafirisha wote kuendelea na safari zao hadi wanapokwenda.
Mganga mfawidhi hospitali ya wilaya ya Uvinza daktari David Patrick amesema wagonjwa sabini na tatu walipokelewa hospitalini hapo siku ya ajali na kuwapatia matibabu, wakati mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa maweni Kigoma, daktari Lameck Mdengo amesema hadi sasa wamebaki wagonjwa wanne kati ya watano waliokuwa wamelazwa.
Kadogosa amesema uchunguzi unafanyika kujua chanzo cha ajali na kusisitiza kugharamikia matibabu kwa majeruhi wote sabini na tatu ili kuwaondolea usumbufu.