Vijana watakiwa kutunza mazingira Kasulu
28 August 2024, 13:51
Ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko, halmashauri ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma imeendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kufanya usafi huku ikiendelea kutoa elimu kwa wananchi waweze kuzingatia usafi wa mazingira.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Vijana kutoka taasisi ya TAYO iliyopo chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Anglikana Kasulu Mjini wamefanya usafi wa mazingira, kutoa msaada wa sabuni na kuchangia damu katika kituo cha afya cha Kiganamo halmashauri ya mji Kasulu ili kuboresha mazingira na kuokoa maisha ya wahitaji.
Vijana hao akiwemo Mwenyekiti wa Idara ya Vijana kanisa kuu Joanita Lumenyela, kaimu katibu wa idara hiyo Sudy Kuyanga na Shemasi Lewina Shimantumwe wameanza na zoezi la usafi ukiwa ni mkakati wao kuhakikisha usafi wa mazingira unazidi kuimarika katika maeneo ya huduma za jamii ambapo wamefanya usafi huo katika kituo cha afya cha Kiganamo.
Mchungaji msaidizi wa kanisa kuu la Mt. Andrea Anglikana Kasulu Mjini Zabron Mdogo amesema hawakuishia kufanya usafi tu bali wameshiriki pia suala la utoaji wa damu salama ili kuokoa maisha ya wahitaji ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali.
Kwa upande wake Daktari Kigwinya Moshi Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kiganamo kilichopo halmashauri ya mji Kasulu amewashukuru kwa namna walivyofika katika kituo hicho na kufanya usafi, uchangiaji wa damu sambamba na kutoa msaada kwa akina mama wajazazito na ambao tayari wameshajifungua.
Naye mwakilishi wa akina mama waliopewa msaada wa sabuni na vijana kutoka kanisa kuu anglikana kasulu Mjini hapa anatoa neno la shukrani.