Imani potofu zahatarisha misitu
20 August 2024, 11:23
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amewataka wananchi wilayani humo kutumia njia sahihi za kuandaa mashamba yao na kuacha tabia ya kuchoma moto misitu wakati wa maandalizi ya kilimo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wilayani humo ambapo amewataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu mazingira kwa kuchoma moto misitu jambo ambalo linaweza kusababisha uharibifu wa kwa kuunguza mazao ya watu shambani
Kanali Ngayalina amesema baadhi ya wananchi wamekuwa na Imani potofu wakihusisha uchomaji moto na maisha yao huku wengine wakifanya hivyo kwa ajili ya chakula cha mifugo.
Aidha Kanali Ngayalina amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaotumia kinyesi cha Ng’ombe kuchoma moto kuwa ni chanzo kikubwa cha kusababisha madhara kwakuwa huacha wameutelekeza moto huo na kusababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo umeme.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wilayani Buhigwe wamesema matukio ya kuchoma misitu yanaongezeka kutokana na kutokuwepo kwa sheria kali dhidi ya wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo na kwamba ikiwa serikali itaweka mikakati ya kuwakamata wanachoma moto misitu itafanikiwa kukomesha suala hilo.