Chakula kwa wanafunzi shuleni kupunguza utapiamlo
15 August 2024, 09:42
Serikali wilayani Kibondo mkoani Kigoma imesema itaendelea kuhakikisha wananchi wanachangia chakula shuleni ili kusaidia kuongeza ufaulu lakini kudhibiti utapiamlo unaotokana na ukosefu wa lishe kwa watoto.
Na James Jovin – Kibondo
Wazazi na walezi wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza juhudu za kuchangia chakula kwa wanafunzi shuleni ili kupunguza idadi kubwa ya watoto wanaoshinda na njaa hali inayowaathiri kiafya na masomo kwa ujumla.
Katika taarifa iliyotolewa na afisa lishe wa wilaya ya Kibondo Bw. Tumaini Muna katika kikao kazi cha kujadili masuala ya lishe wanafunzi wanaopata chakula shuleni kwa mwaka ni asilimia 66 pekee hali ambayo inakwamisha juhudi za serikali katika kumaliza magonjwa ikiwemo utapiamlo.
Kwa upande wake afisa tarafa wa tarafa ya Kifura Bw. Shekarata Omary amesema kuwa lishe inapaswa kuwa ajenda ya kudumu katika vikao mbalimbali ikiwa ni sambamba na kuwahamasisha wazazi na walezi kuongeza bidii katika kuchangia chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao.
Kwa upande wake Bw. Steven Janks akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji katika kikao hicho amewataka watendaji kutumia sheria ndogo zinazohusu masuala ya chakula shuleni ili kuongeza idadi ya Watoto wanaokula chakula shuleni na hivyo kupunguza magonjwa ikiwemo utapiamlo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza amewataka viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanabaini changamoto mbalimbali zinazopelekea wazazi kushindwa kuchangia chakula shuleni na kuzifanyia kazi ili kuweza kupunguza ama kumaliza kabisa tatizo hilo.