Mbunge atoa msaada wa mabati kujenga ofisi CCM
1 August 2024, 11:57
Katika kuunga mkono juhudi za ujenzi wa ofisa ya chama cha mapinduzi wilayani buhigwe, Mbunge wa Jimbo hilo ametoa mabati ili kuanza ukarabati wa ofisi hiyo.
Na Tryphone Odace – Buhigwe
Mbunge wa jimbo la Buhigwe Mkoani Kigoma Felix Kavejuru ametoa msaada wa bandari 12 za bati kwa ajili ya kusaidia kumalizia ujenzi ya ofisi ya CCM ya wilaya hiyo.
Kavejuru amekabidhi bati hizo zenye thamani ya shilingi milioni 5.9 kwa Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi ya ofisi hiyo,Silvestre Kigwinya na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa CCM wilaya Buhigwe.
Mbunge huyo alisema kuwa msaada huo aliotoa ambao umelenga kuunga mkono juhudi za viongozi wa wilaya hiyo kuwa na ofisi yao yenye hadhi ya wilaya kuondoka katika jengo la kuazima ambalo wanalitumia sasa.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya kamati ya ujenzi, Mwenyekiti wa kamati hiyo Silvestre Kigwinya ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Buhigwe alisema kuwa msaada huo utawezesha mradi wa ujenzi wa ofisi hiyo kupiga hatua kubwa.
Kigwinya amemshukuru Mbunge huyo wa jimbo la Buhigwe kwa kujitoa kwake akiamini kwamba baada ya hatua hiyo mipango ya kufanya usafi na kukamilisha jengo haitachukua muda mrefu ili kuwezesha ofisi hizo kutumika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya Buhigwe, Erneo Dyegula amemshukuru Mbunge Kavejuru kwa msaada huo wa mabati kuunga mkono juhudi za ujenzi wa jengo hilo la ofisi ya CCM wilaya Buhigwe kwani litawafanya kuwa na ofisi yao kuondoka katika ofisi ya kuazima ya CCM kata ya Buhigwe ambayo wanatumia sasa.
Dyegula alisema kuwa wilaya hiyo ambayo ni moja ya wilaya tatu mpya mkoani Kigoma imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa majengo kwa matumizi ya ofisi hivyo kulazimika kujiazima katika baadhi ya majengo ya kata au nyumba za kupangisha.