Wananchi watakiwa kulinda miradi ya maji
31 July 2024, 12:41
Serikali kupitia kwa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma imesema wananchi wamekuwa wakishindwa kutunza na kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na shinikizo la itikadi za vyama vya siasa.
Na Michael Mpunije – Buhigwe
Wananchi wilayani Buhigwe mkoani Kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kukataa miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao kwakuwa miradi hiyo inakuwa na lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Ruwasa wilaya ya Buhigwe injinia Golden gwakatoto wakati akizungumza na kipindi hiki.
Injinia Golden amesema baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kukataa miradi inayotekelezwa na serikali kutokana na itikadi za Kisiasa katika baadhi ya maeneo wilayani Buhigwe jambo ambalo linachelewesha maendeleo ya wananchi na kushindwa kutatua baadhi ya changamoto za maji kwa wakati huku akiwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha injinia Golden amesema maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya maji kutokana na geografia ya maeneo hayo bado upo mpango wa serikali wa kuhakikisha wananchi wa Buhigwe wanapata maji safi na salama ambapo ameeleza pia katika utekelezaji wa miradi ya maji wamelenga kufikisha huduma hiyo katika maeneo ya taasisi mbalimbali ikiwemo,soko,shule na vituo vya kutolea huduma za afya.