Joy FM

Zaidi ya familia 300 zapewa msaada wa chakula Uvinza

26 July 2024, 13:16

Mkurugenzi wa shirika hilo la Hope of the nations Bw. Horold Knepper akiwa anakabidhi msaada wa chakula, Picha na Mullovan Chepa

Wananchi wa kijiji cha Lyabusenda kata ya Sunuka wilayani Uvinza ambao ni miongoni mwa wanaopitia kipindi kigumu baada ya shughuli za uvuvi kusitishwa ziwa Tanganyika na kusababisha kipato kuyumba wameomba wadau wa maendeleo kuwasaidia kuwapa misaada ili kujikimu kimaisha.

Na Timotheo Leonard – Uvinza

Shirika la kidini linalojishughulisha kufundisha  neno la Mungu na maendeleo la Hope of the Nations limetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mchele kilo 1,000 na maharage kilo 500 kwa wananchi wa kijiji cha Lyabusende kata ya Sunuka wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, mkurugenzi wa shirika hilo la Hope of the Nations Bw. Horold Knepper amesema wameamua kutoa msaada huo baada ya kuona wakazi wa eneo hilo wana uhitaji wa mahitaji mbalimbali.

Sauti ya mkurugenzi wa shirika la Hope of the Nations

Tupo hapa kwa ajili ya kuwasaidia watu ambao wanasumbuka kupata chakula wakati mwingine kutokana na sababu za kitega uchumi chao cha uvuvi kupumzishwa na leo tumetoa msaada wa kilo 1,000 za mchele na kilo 500 za maharage ili kuwezesha takribani familia miatatu.”

Mkurugenzi wa shirika hilo la Hope of the nations Bw. Horold Knepper akiwa anakabidhi msaada wa chakula, Picha na Mullovan Chepa

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lyabusende kata ya Sunuka Bw. Michael  Venance amelishukuru shirika hilo  kwa kuwapatia msaada wa mchele na maharage wananchi ambao anaamini utawasaidia kujikimu kimaisha.

Sauti ya afisa mtendaji wa kijiji cha Lyabusende kata ya Sunuka Bw: Michael  Venance

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake Bi. Anna Raymond amelishukuru shirika hilo kwa kuona kuwa wanapitia wakati mgumu na wanahitaji msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula.

Sauti ya wananchi wenzake Bi. Anna Raymond
Mkurugenzi wa Hope of the Nationa akiwa na wananchi baada ya kuwapatia msaada, Picha na Mullovan Chepa