KUWASA yapewa heko utatuzi wa kero ya maji
19 July 2024, 08:53
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira manispaa ya Kigoma Ujiji (KUWASA) imesema imeendelea kuboresha miundombinu ya usambazaji wa maji kwenye makazi ya watu ili kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha.
Na Emmanuel Matinde – Kigoma
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Kigoma, kimeeleza kuridhishwa na kupongeza kazi inayofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma Ujiji (KUWASA), ya kutatua kero ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM ambapo kamati hiyo ya siasa imetembelea miradi mbali mbali ukiwemo mradi wa ujenzi wa uboreshaji wa kitekeo cha maji katika eneo la Kibirizi ambacho kitasukuma maji kwenda kwa wananchi wa kijiji cha Kalalangabo.
Uwezo mdogo wa kuzalisha maji katika chanzo cha maji cha awali eneo la Kibirizi umesababisha wakazi wa kijiji cha Kalalangabo kukosa huduma ya maji safi na salama, kwa hivo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Kigoma Ujiji KUWASA, inatekeleza mradi wa maji utakaopunguza kero hiyo kwa wananchi.
Kamati ya siasa baada ya kukagua mradi huo imepongeza jitihada zinazofanywa za kumtua mwanamke ndoo kichwani.
Kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 80% ya utekelezaji wake lakini kwa kiasi wakazi wa kijiji cha Kalalangabo, wameanza kupata huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo ya kijiji.
Kwa sasa upatikanaji wa huduma ya maji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji umefikia asilimia 92% lengo likiwa ni kufikia asilimia 95% ifikapo mwaka 2025.