Wakulima watakiwa kupima afya ya udongo kigoma
17 July 2024, 16:12
Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kutambua namna ya kupima afya ya udongo ili waweze kulima kilimo chenye tija na ushindani kwenye sokola ndani na nje ya nchi.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Wakulima wa mazao mbalimbali Mkoani kigoma wametakiwa kupima afya ya udongo kabla ya kuanza zoezi la upandaji wa mazao ili kufuata hatua za kilimo bora katika kukabiliana na changamoto ya uvunaji mdogo wa mazao.
Hayo yameelezwa na meneja wa shirika Nyakitonto Youth development Tanzania Bw.Elvas mbogo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa kilimo kutoka katika halmashauri za mkoa wa Kigoma pamoja na baadhi ya wauzaji wa pembejeo za kilimo kutoka mkoani humo ambayo yamefanyika mjini Kasulu.
Bw.Mbogo amesema ili kuvuna mazao mengi ni muhimu wakulima kupima afya za udongo katika mashamba yao kabla ya kupanda pamoja na kutumia chokaa ya kilimo ambayo husaidia kurejesha rutuba kwenye udongo kutokana na mashamba mengi ya wakulima kuonekana kuwa yameathiriwa na asidi.
Kwa upande wake afisa kilimo kutoka halmshauri ya wilaya ya kibondo bw.Martine Msabila amesema wameshaanza zoezi la upimaji wa afya udongo kwenye mashamba ya wakulima pamoja na kutoa elimu kuhusu chokaa ya kilimo wakati huo afisa kilimo kutoka halmashauri ya wilaya ya Kasulu akieleza kuwa bado mwitikio wa wakulima kupima afya za udongo katika mashamba yao bado ni mdogo kutokana na kuwa na imani potofu kuhusu vipimo hivyo.
Aidha baadhi ya wauzaji wa pembejeo za kilimo wameishauri serikali kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kupima afya ya udogo wakati wa shughuli za kilimo pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi sahihi ya chokaa ya kilimo.