Joy FM

“Wizara ya nishati unganisheni Kigoma na gridi ya taifa”

9 July 2024, 09:26

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango, Picha na OMR

Mkoa wa kigoma bado unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo ambalo limekuwa vigumu hata kwa wawekezaji wakubwa kuvutiwa kuja kuwekeza kwenye mkuu huu hali ambayo serikali imeamua kutatua changamoto hiyo kwa kuunganisha mkoa huu na gridi ya Taifa.

Na Josephine Kiravu – Kigoma

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa ifikapo Septemba, mwaka huu, mkoa mzima wa Kigoma uwe umeungwa na Gridi ya Taifa.

Dk Mpango amesema hayo alipotembelea kituo cha kupoza umeme cha Nguruka ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 95.

Amesema Kigoma ni moja ya mikoa inayokabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umemewa uhakika, hali inayorudisha nyuma uwekezaji na maendeleo yake.

 Amesema suluhisho lililobaki  ni mkoa huo kuungwa na Gridi ya Taifa, huku akisema katika hilo hana shaka litatekelezwa kwa sababu waziri mwenye dhamana, Dk Doto Biteko na naibu wake, Judith Kapinga ni wachapa kazi.

Umeme wa gridi ya Taifa kuingia kigoma kunatajwa kuwa mkombozi wa wananchi, Picha na Mtandao

“Niipongeze hii wizara kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya sekta ya nishati, hususan miradi ya umeme ambayo inaifanya nchi sasa ijiimarishe kiuchumi,” amesema Dk Mpango.

Mbali ya kukagua kituo hicho, Makamu wa Rais, yupo mkoani Kigoma kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilomita 395.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Kapinga ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali, hususan wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nguruka.

Kapinga amesema Wizara ya Nishati itaendelea kusimamia miradi yote na kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika kwa wananchi.

“Nikuhakikishie Mheshimiwa Makamu wa Rais, sisi Wizara ya Nishati hatutakuwa kikwazo kwa wananchi kupata umeme, bali tunaahidi kuwapatia umeme wa uhakika Watanzania wote,” amesema Kapinga.

Amesema miradi yote ya umeme ya kimkakati wizara itahakikisha inaisimamia, ukiwamo wa Igamba Kidahwe hadi Malagarasi ambao mpaka sasa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi.

Ikumbukwe mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kigoma na kituo cha kupoza umeme cha Nguruka, unatekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya TBEA kutoka China na unagharimu zaidi ya Sh12 bilioni na ujenzi wa kituo  cha kupoza umeme cha Kidahwe kitakachopokea umeme kutoka  Nyakanazi, unagharimu Sh5 bilioni, unatekelezwa na wataalamu wa ndani kutoka Tanesco.

Wananchi wa kata ya nguruka wakimsikiliza makamu wa Rais wa Tanzania katika mwendelezo wa ziara yake, Picha na OMR

Ujenzi huo ukikamilika utaunganisha wilaya nne za Mkoa wa Kigoma ambazo ni Kigoma Mjini, Buhigwe, Uvinza na Kasulu na pia kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme kwa mkoa kupitia Gridi ya Taifa.

Baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kigoma liunganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa Septemba 2022, lakini hadi sasa haukuwa umefika maeneo yote.