Umeme wa gridi ya taifa kuifungua Kigoma
3 July 2024, 14:21
Serikali ya mkoa wa Kigoma imesema dhamira ya serikali kuu ni kuona Kigoma inakuwa na umeme wa uhakika ili kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Na Sadiki Kibwana – Kigoma
Jumla ya shilingi bilioni 434 zilizotolewa na serikali zimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya nishati ya umeme wenye kilovati 400 ili kuondoa changamoto za upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mkoa wa Kigoma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye, wakati akizungumza na Joy Fm na kueleza miradi mbalimbali inayojengwa na serikali mkoani hapa.
Mh. Andengenye amesema hayo yamefanyika ili kuutoa mkoa wa kigoma kwenye giza ambapo umeme huo unaotoka Nyakanazi mpaka Kidahwe unatarajiwa kupokelewa tarehe 30 mwezi huu huku umeme wa kutoka Tabora kwenda Nguruka wenye kilovati 132 unatarajiwa kuongezeka kwenye gradi ya Taifa.
Wakati huo huo, Mhe Andengenye amesema Benki ya dunia imetoa mkopo kwa Tanzania ili kigoma iweze kuzalisha umeme katika kijiji cha Igamba kutoka mto malagarasi ambapo mradi huo utazalisha megawati 49.9 ambazo zitaingia katika gradi ya taifa na kuongeza upatikanaji wa umeme.
Katika hatua nyingine Mhe. Andengenye amesema upatikanaji wa Nishati ya umeme utasaidia mkoa wa kigoma kufungua fursa mbalimbali ikiwemo maendeleo ya kibiashara na viwanda.