Volkano la tope lalipuka, hofu yatanda kwa wananchi Kigoma
2 July 2024, 16:28
Serikali katika halmashauri ya wilaya Kigoma imewataka wananchi kutulia wakati ikiendelea kufuatilia hali ilivyo baada ya volkano la tope kulipuka.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Wananchi wa kijiji cha Pamila kata ya Matendo wametakiwa kuondoa hofu kufuatia kuwepo kwa tope ambalo limechanganyika na maji katika eneo la bonde la mto Nyankara huku wengine wakidhani huenda ikawa ni aina ya volkano.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli amefunga safari hadi eneo hilo kwa ajili ya kujionea hali halisi ambapo amewataka wananchi kuwa watulivu na kuziachia mamlaka husika kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusu hali hiyo.
Kwa upande wake Edith Makungu ambaye ni Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka ofisi ya mazingira NEMC amewataka wananchi kwa muda huu kukaa mbali na eneo hilo ambalo ni kwa muda huu linaonekana kuwa na madhara.
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Pamila Peter Hungu amesema hali hiyo kwa mujibu wa wananchi imeanza kuonekana takribani miezi miwili iliyopita na kwamba eneo hilo lilikuwa ni maalum kwa ufugaji wa samaki.