“DC kibondo wanawake wanafanyiwa ukatilii hawasemi”
12 June 2024, 12:09
Katika kukabiliana na vitendo vya ukatilii na unyanyasaji kwa wanawake na watoto, wadau na serikali wametakiwa kuungana kwa pamoja kushughulikia ukitilii dhidi ya vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikiacha kovu na huzuni miongoni mwa wahanga wa matukio hayo.
Na James Jovin – Kibondo
Shirika lisilo la kiserikali Kibondo Paralegal Foundation (KIPAFO) wamezindua mradi wa majaribio MWANAMKE SALAMA wenye dhumuni kupambana na ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Kibondo na kuongeza juhudi za kutetea haki za wanawake na kukuza utu wao katika jamii.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mradi huo kutoka shirika la KIPAFO bw. Mussa Mashishanga wakati wa uzinduzi wa mradi huo mbele ya mkuu wa wilaya ya Kibondo kanali Agrey Magwaza na wadau wa mradi huo
Bw. Mashishanga amesema kuwa mradi huo utatekelezwa katika kata tano ndani ya wilaya ya Kibondo na kushughulikia ukubwa wa matatizo, matokeo na changamoto zinazohusiana na unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika la KIPAFO wilayani Kibondo bw. Japhet Razalo amewataka viongozi katika kata zilizochaguliwa wakiwemo madiwani na watendaji kutoa ushirikiano katika shughuli hiyo ili kusaidia kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na wasichana.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kibondo kanali Agrey Magwaza amewataka wadau wote wa mradi wa Mwanamke salama wakiwemo viongozi wa dini kuwa vinara wa kupinga ukatili wa kijinsia hali itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza tatizo hilo ndani ya jamii.