Ukosefu wa mbolea kikwazo kwa wakulima wa tumbaku
11 June 2024, 12:16
Wakulima wa zao la tumbuku nchini tanzania wameiomba serikali kusimamia suala la utoaji wa mbolea ili ziweze kutoka mapema ili waweze kuendana na msimu wa kulimo hicho ambacho kinaonekana uzalishaji wake kuongezeka.
Na Emmanuel Matinde – Kigoma
Imeelezwa kuwa licha ya jitihada zinazofanywa na wakulima, uzalishaji wa tumbaku nchini unaweza kuzorota na kukosa tija kwa mkulima endapo suala la ucheleweshaji wa pembejeo hasa mbolea halitapatiwa ufumbuzi madhubuti wa kudumu.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita uzalishaji wa tumbaku nchini umeongezeka kutoka tani elfu 37 hadi kufikia tani laki moja na elfu 25 kufuatia mipango ya serikali ya kuvutia wawekezaji ambayo imechochea ongezeko la wanunuzi wa tumbaku na hivyo mahitaji na bei ya pia kuongezeka na wakulima kuanza kuchangamkia fursa hiyo.
Hata hivyo katika misimu miwili iliyopita kilio cha wakulima wa tumbaku kimekuwa ni ucheleweshaji wa pembejeo hasa mbolea hali inayowaibua wakulima kupaza sauti wakitaka misimu inayofuata mbolea ifike kwa muda muafaka.
Kuelekea msimu wa kilimo 2024/2025 tayari serikali imeipa jukumu la usambazaji wa mbolea kwa wakulima Kampuni ya Mbolea Tanzania TFC, pamoja na kutangaza kuweka ruzuku kwenye mbolea, kama wanayoeleza Mkurugenzi wa TFC Samuel Mshote na Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Stanley Mnozya.
Yote hayo yamejiri kwenye mkutano wa sita wa mwaka wa Mradi wa Pamoja wa Wakulima wa Tumbaku Tanzania TCJE, uliofanyika mkoani Kigoma, ambapo Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Juma Mokili, ameitaka TCJE kusimamia kanuni za kilimo bora cha tumbaku.