DC Kigoma aagiza kero ya umeme kutatuliwa
28 May 2024, 14:43
Licha ya serikali ya kusema kuwa hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni nzuri bado hali ya upatikanaji wa umeme mkoa wa kigoma umekuwa sio wa uhakika kutokana na kutolewa kwa mgao.
Na Josephine Kiravu – Kigoma
Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli ametembelea kituo cha kuzalisha na kupoza umeme hapa mkoani Kigoma na kujionea namna uzalishaji unavyofanyika na kuitaka TANESCO kuangalia upya mgao wa umeme unaoendelea hivi sasa hasa inapofika nyakati za usiku.
Awali akisoma taarifa ya upatikanaji wa nishati ya umeme, Meneja wa TANESCO mkoa wa kigoma Julius Mtei Sabu amesema mara kadhaa kituo hicho cha uzalishaji kimekuwa kikizidiwa kutokana na kuhudumia watu wengi ambapo kwa mwezi hutumia kiasi cha zadi ya billion 1.6 kwa ajili ya kununua mafuta huku fedha wanazokusanya ni bilioni 1.6 kutoka kwa wateja.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya kigoma akiwa katika ziara hiyo ya kufanya ukaguzi kwenye ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme pamoja na eneo la uzalishaji nishati hiyo ametoa ushauri kwa Meneja wa TANESCO kuona haja ya kurekebisha mgao wa umeme licha ya kuwa yapo maeneo ambayo nishati hiyo inapaswa kupatikana muda wote.
Naye Mhandisi wa Tanesco Mkoa wa kigoma Karim Namahale amesema changamoto za uzalishaji wa umeme mkoa wa kigoma ni mgumu kutokana kutegemea umeme wa sola ambao uzalishaji wake huishia jioni tu hali kusababisha umeme kuwa pungufu.
Baadhi ya wananchi mkoani kigoma wamesema kuwa hali ya upatikanaji wa umeme ni mbaya kwani muda mwingi hakuna umeme hali inayosababisha shughuli za maendeleo kushindwa kufanyanyika ikiwemo watu wenye viwanda vidogo na vya kati.
Kwa mujibu wa meneja, miradi inayotekelezwa mpaka hivi sasa ni mitatu ambayo inagharimu kiasi dola million 186.93 na ikikamilika inatajwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo ndani ya wilaya ya kigoma ambyo mpaka sasa inahudumia wateja 37,827 pamoja na viwanda vikubwa na vidogo 19.