“Wananchi acheni kuhujumu miundombinu ya umeme”
28 May 2024, 11:29
Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO mkoani Kigoma limewataka wananchi kutoa taarifa za watu wanaoharibu miundombinu ya umeme kwa kukata nyaya na kuchoma moto nguzo za umeme.
Na Michael Mpunije – Kasulu
Wananchi wilayani Kasulu Mkoani kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme kutokana na kuibuka kwa tabia ya wizi wa nyaya za umeme katika maeneo mbalimbali wilayani kasulu.
Akizungumza na Radio Joy ofisini kwake Meneja wa TANESCO wilaya ya Kasulu mhandisi Danford Yungu amesema kumekuwepo na tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme jambo ambalo limekuwa likiathiri maendeleo ya wananchi.
Amesema wananchi wanatakiwa kuwa walinzi wa miundombinu hiyo ili kuendelea kuleta maendeleo kupitia nishati ya umeme.
Aidha mhandisi Danford ameliomba jeshi la polisi kuendelea kufuatilia na kubaini wanaojihusisha na wizi wa nyaya za umeme ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria sanjari na kuwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.