Kasulu watakiwa kusaidia wanafunzi wenye ulemavu
20 May 2024, 13:59
Wadau wa maendeleo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kujitokeza na kuwasaidia wanafunzi ambao ni walemavu ili kuwawezesha nyenzo mbalimbali zitakazowasaidia kusoma kwa urahisi na kufikia ndoto zao.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya serikali katika sekta ya elimu, kikundi cha wanawake Itunze Thamani Yako (ITY) kutoka halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma kimetoa msaada wa kitimwendo (wheel chair) kwa Stanley Jonathan mwanafunzi mwenye ulemavu wa miguu chenye thamani ya shilingi laki 8 kutoka katika shule ya msingi Kasulu.
Akizungumza kabla ya kumkabidhi kiti hicho, mwenyekiti wa ITY Imani Makarabo amesema lengo la kutoa msaada huo ni kutokana na changamoto aliyonayo mtoto huyo na msaada huo utamsaidia katika kumtia moyo ili aweze kutimiza malengo yake.
“Baada ya kutambua uwepo wa mtoto huyu katika shule hii ya Kasulu tumeamua kuchangishana na kununua kitimwendo hiki ili kiwe msaada kwa mwanafunzi huyu aweze kufikia ndoto zake”
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kasulu Rose Kibindi amewashukuru wanawake wa kikundi hicho kwa msaada walioutoa kwa mwanafunzi wake, huku akiomba msaada zaidi jamii kufuatia uwepo wa wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum shuleni hapo.
Aidha afisa elimu kata ya Murusi Gervas Lugeze ambaye amemuwakilisha afisa elimu, elimu ya watu wazima halmashauri ya Mji Kasulu amesema katika kata hiyo wapo wanafunzi wenye uhitaji maalum hivyo amewaomba kuendelea kutoa msaada hata katika maendeo mengine ambayo kuna wanafunzi wenye changamoto za namna hiyo.
Naye Frida Saidi Mama mzazi wa Stanley Jonathan licha ya kukishukuru kikundi cha Itunze thamani yako amesema Stanley alizaliwa bila tatizo lolote lakini alipofika darasa la nne ndipo magonjwa yakaanza kumuandama huku familia yake ikijitahidi kumsaidia kwa kumpeleka hosptitali mbalimbali ili kupata matibabu lakini hakuna mafanikio yoyote aliyoyapata mtoto huyo.