Joy FM

DC Kasulu: Wakulima msiuze mazao kiholela

10 May 2024, 16:00

Mkuu wa wilaya kasulu akizungumza katika baraza la madiwani, Picha na Hagai Ruyagila

Katika kukabiliana na njaa pamoja na uhaba wa chakula serikali imewahimiza wakulima kuhakikisha hauwazi mazao kiholela.

Na Hagai Ruyagila

Wakulima wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuepuka kuuza mazao yao ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa chakula.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kasulu kanal Isaac Mwakisu wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Kasulu.

Katika kikao hicho cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024 Kanal Mwakisu amewasihi wakulima kutouza chakula walichonacho kutokana uchache wa chakula uliopo katika wilaya hiyo kufuatia mvua zilizonyesha na kusababisha mazao kuharibika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Eliya Kagoma ambaye pia ni diwani wa Kata ya kitanga amemsihi mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na Watendaji wa kata zote kuhakikisha wanaziba mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha ili kuthibiti mapato na kuvuka lengo walilijiwekea.

Nao baadhi ya madiwani wa kata zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu akiwemo diwani wa kata ya Bugaga Hitra Mlobelo na diwani wa kata ya Asante Nyerere Julius Mpwehuka wamesema wako tayari kuzungumza na wananchi ili wasiuze chakula ili waweze kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa chakula.

Madiwani wilayani kasulu wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani, Picha na Hagai Ruyagila