Joy FM

RC Andengenye awataka vijana wa jkt kujiajiri

6 May 2024, 08:53

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye akikagua gwaride la vijana wa JKT Mtabila, Picha na Tryphone Odace

Vijana wa kujenga wanaohitimu mafunzo ya kijeshi katika kambi ya mtabila wametakuwa kuwa wazalendo kwa nchi na kutumia maarifa na ujuzi waliopata katika kujiajiri na kuacha kutegemea ajira.

Na, Tryphone Odace – Kasulu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutumia ujuzi waliopata kujiajiri kwakuwa Tanzania hakuna changamoto ya kazi ingawa kuna changamoto ya ajira.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi ya vijana wa kujitolea Operesheni miaka 60 ya JKT katika kikosi cha Jeshi 825 Mtabila iliyopo wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Mkoa huyo amesema kupitia mafunzo hayo jeshi linajivunia kuwa na jeshi la akiba imara na hodari na matunda ya kazi hiyo ni kuona taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu na kuwa viongozi wenye kulipenda taifa na ndio msingi wa kiapo chao.

“Mafunzo mliyoyapata nendeni mkayatumie vizuri ili kutimiza lengo kuwaanda jeshi la akiba na kamwe msikubali mtu yeyote awalaghai na mkajiunga na vikundi vya uhalifu kwani huo utakuwa ni usaliti wa kiapo chenu na usaliti kwa taifa,” amesema Andengenye.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akikagua gwaride la vijana wa JKT Mtabila wilayani Kasulu,Picha na Tryphone Odace

Kiongozi huyo pia amewaasa wahitimu hao kutokubali kulaghaiwa na kujiunga na vikundi mbalimbali vya kihalifu, kwani kukubali kulaghaiwa ni usaliti wa kiapo cha jeshi na usali kwa taifa ambalo limetumia gharama kubwa kuwaandaa.

Kwa upande wake Muwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Tawi la Ugavi, Uchukuzi na Uhandisi Makao Makuu ya Jeshi, Meja Jenerali Hawa Kodi amewataka vijana hao kutumia jukwaa hilo kuwaelimisha wengine kwa vitendo kuwa wao ni wazalendo na kujiepusha vitendo vitakavyowaingiza kwenye matatizo ya afya ya mwili na afya akili.

“Afya ya akili ndio msingi mkubwa wa maisha yenu nendeni mkazingatie yote mlijifunza bila kusahau kuchukua tahadhari ya kujiepusha na magonjwa yanaambikiza”

Vijana wa JKT Mtabila wakionyesha ukakamavu wao wakati wa kufunga mafunzo ya vijana wa kujitolea kwa mujibu wa sheria oparesheni miaka sitini ya JKT, Picha na Tryphone Odace

Naye, Mwakilishi wa Mkuu wa JKT, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kufuatia mafunzo hayo vijana hao watakuwa tayari kutumikia na kulilinda taifa popote watakapokuwa na kuwataka kutumia elimu waliyoipata katika kutatua changamoto mbalimbali pasipo kuvunja sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Mwakilishi wa Mkuu wa JKT, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, Picha na Tryphone Odace