Wananchi kufikishwa mahakamani waliohujumu eneo la uwekezaji
2 May 2024, 12:25
Serikali wilayani kibondo imesema itaendelea kuwachukulia hatua wanaokiuka taratibu za uwekezaji kwa kuvamia maeneo yanayokuwa yamepangwa kwa ajili ya uwekezaji.
Na James Jovin – Kibondo
Halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma inapanga kuwaburuza mahakamani baadhi ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka bonde la mto Rumpungu wanaohujumu maeneo yaliyopimwa na serikali kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha biashara
Hayo yamebainishwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo bw. Deocles Rutema wakati wa kikao cha kuwasilisha utekelezaji wa Ilani mbele ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo.
Aidha amesema kuwa serikali ilitumia zaidi ya shilingi milioni 100 kupima eneo hilo la uwekezaji lakini baadhi ya wananchi wanaozunguka eneo hilo wamekuwa wakivuruga mpango huo licha ya makubaliano ya awali kuwa wanapaswa kuondoka katika eneo hilo ili kupisha mwekezaji kwa masirahi ya umma.
Katika hatua nyingine bw. Rutema amewataka wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mto Rumpungu kuwapa maeneo mengine wananchi wanaodai kuwa walichukuliwa ardhi yao ili kupisha mwekezaji atakayepata ridhaa ya kuwekeza katika eneo hilo
Kwa upande wake mwenyekiti wa ccm wilaya ya Kibondo bw. Hamisi Tahilo amesema kuwa maendeleo yoyote ni lazima yaache maumivu kwa baadhi ya wananchi ili kunufaisha jamii nzima hivyo ni vema wananchi hao wakapisha mwekezaji kwa manufaa ya jamii nzima.