Acheni kunyanyasa wafanyakazi katika maeneo ya kazi
1 May 2024, 15:13
Wafanyakazi wa sekta mbalimbali leo wameadhimisha siku ya wafanyakazi huku wakiomba serikali kupitia vyama vya wafanyakazi kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali mstaafu wa Jeshi la Zimamto na uokoaji Thobias Andengenye,ameviagiza vyama vya wafanyakazi kutatua changamoto zilizopo baina ya waajiri na wafanyakazi wao ili kuongeza ufanisi wa kufanya kazi kwa weledi.
Ametoa maagizo hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanya kazi duniani ambayo kwa Mkoa wa Kigoma yamefanyika wilayani kasulu katika uwanja wa umoja.
Aidha Andengenye amesema kumekuwepo baadhi ya Taasis na mashirika ambayo yamekuwa yakiwanyanyasa wafanyakazi jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo kwa wafanyakazi.
‘mfanyakazi hauwezi kuwa na uhuru wa kufanya kazi kwa weledi kama hapewi uhuru maana wengi wamekuwa wakinyanyaswa na waajiri wao lakini pia hata wakuu wao wa kazi jambo ambalo linarudisha nyuma morali kwa wafanyakazi”
kwa upande wake Katibu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Kigoma TUCTA bw.Jumanne Hamisi magulu amesema katika risala kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ijitathimini kwakuwa baadhi ya waajiri hawapeleki michango ya wafanyakazi kwa wakati na kusababisha usumbufu huku akiitaka Serikali kuangalia namna ya kurejesha mishahara halisi pale mtumishi anapostaafu
Aidha baadhi ya wafanyakazi Mkoani Kigoma wamesema ikiwa changamoto hizo zitatuliwa kwa wakati zitasaidia kukuza maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho ya siku hii ya wafanyakazi kimkoa yamefanyika hapa katika viwanja vya umoja Kasulu na Kitaifa ni kule Jijini Arusha yakiwa yamebebwa na kauli mbiu isemayo nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao Bora na kinga dhidinya Hali ngumu ya maisha